SALAMU KUTOKA KWA BALOZI
Kwa furaha ninawakaribisha kwenye tovuti rasmi ya Ubalozi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Falme ya Netherlands. Ubalozi unashughulikia
masuala ya uwili na Kimataifa. Katika uwili Ubalozi unaiwakilisha Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Falme ya Netherlands, ambayo inajumuisha nchi nne
zinazojitawala ikiwemo Netherlands yenyewe na nchi tatu za Aruba, Curacao na St.
Marteen, zilizoko Karibiani.
Kimataifa Ubalozi unaiwakilisha Tanzania katika Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali
(OPCW), Mfuko wa Mazao Duniani (CFC), Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ),
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), na taasisi nyingine za kisheria za kimataifa
zenye makazi katika Falme ya Netherlands.
Jukumu kubwa la Ubalozi ni kuimarisha na kukuza uhusiano uliopo kati ya Tanzania
na Netherlands. Kwa kuwa dira ya sasa ya Tanzania ni utekelezaji wa Diplomasia ya
Uchumi kama msukumo mkuu wa Sera yake ya Mambo ya Nje, Ubalozi una jukumu
la kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo bora ya uwekezaji, utalii na biashara.
Ubalozi una wajibu wa kusimamia haki za raia wa Tanzania walioko Netherlands
wanaojumuisha Diaspora na wanafunzi katika kutekeleza dira hii ya maendeleo na
nchi kwa ujumla.
Amani na utulivu wa Tanzania tangu ilipopata uhuru (1961),ni ujumbe wa matumaini
kwa wawekezaji watarajiwa, washirika wa biashara, marafiki na wageni kutoka
pande zote za dunia. Tanzania ni nyumbani kwa maeneo matatu mashuhuri ya utalii
- mlima mrefu zaidi barani Africa: Kilimanjaro, kisiwa cha marashi ya karafuu cha
Zanzibar, na mbuga za wanyama za asili zaidi ya kumi na sita (16) zikiwemo Bonde
la Ngorongoro, Serengeti, Tarangire, Arusha, Selous, Kitulo almaarufu bustani ya
Mungu. Hakika Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili nyingi, maziwa na mito ya
kuvutia sana.
Mbali na utajiri wa ardhi ya wanyamapori, kilimo na misitu, Tanzania pia ina utajiri
mkubwa wa madini kama tanzanite, almasi, dhahabu, chuma, makaa ya mawe,
nikeli, urani, mafuta na gesi asilia.
Ni matumaini yangu kuwa tovuti hii inawapa fursa ya kuielewa vyema nchi yetu,
Tanzania, maarufu kwa jina la “THE LAND OF KILIMANJARO”.
Karibuni sana kutembelea Tanzania,
Karibuni sana kuwekeza Tanzania,
Karibuni sana kushirikiana na Tanzania.
Caroline Kitana Chipeta
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu OPCW.