Tarehe 03 hadi 07 Septemba 2022, Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.), Waziri wa Nishati alifanya ziara nchini Uholanzi kumwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Africa Adaptation Summit: High Level Dialogue for the 27th session of the Conference of the State Parties (COP27) uliondaliwa na Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Kituo cha Kukabiliana na Tabianchi (Global Center on Adaptation - GCA). Mkutano huo ulioongozwa (moderator) na Prof. Patrick Verkooijen, Afisa Mtendaji Mkuu wa GCA, ulifunguliwa kwa hotuba za Viongozi Wakuu wakiongozwa na Mhe. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa na pia Mwenyekiti wa Kituo cha GCA na Mhe. Macky Sall, Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Mkutano huo ulifungwa na Mhe. Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Uholanzi. 

Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kuwashawishi Washirika wa Maendeleo, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa ya Kifedha, Sekta Binafsi na Marafiki wa Afrika kuchangia fedha katika Programu ya kukabiliana na majanga kwa nchi za Afrika (African Adaptation Acceleration Program – AAAP) ambayo inahitaji Dola za Marekani Bilioni 25 ifikapo Mwaka 2025. Majanga hayo ni pamoja na madhara yaliyotokana na janga la UVIKO19 na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. Katika ushawishi huo, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imechangia Dola za Marekani bilioni 12.5 sawa na takribani Shilingi trilioni 29, Serikali ya Ufaransa itachangia Euro bilioni 1 sawa na takribani trilioni 2.9. Aidha, Sekta binafsi zimetoa ahadi mbalimbali za kuchangia programu hiyo.

Mkutano huo umefanyika kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi (Conferences of Parties 27 – COP27) ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 4-18 Novemba, 2022 huko Sharm El Sheikh, Misri ambako suala la kuhimili mabadiliko ya Tabianchi kwa Afrika ni moja ya ajenda muhimu ya mkutano huo.