Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii (Holiday Fair 2020) au “Vakantiebeurs 2020” kwa lugha ya Kidachi yameanza rasmi mjini Utretch, Uholanzi. Maonyesho haya na ambayo hufanyika mwezi Januari kila mwaka, yanajumuisha mataifa mbali mbali duniani kutangaza na kuuza vivutio vyao vya Utalii na Burudani kutoka katika nchi zao.

Maonyesho ya “Vakantiebeurs 2020” yameanza rasmi tarehe 16 na yanatarajia kumalizika tarehe 19, Januari, 2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki katika maonyesho haya na imewakilishwa rasmi na wawakilishi kutoka Tanzania Tourist Board (TTB), Tanzania National Parks Authority (TANAPA) na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA); pamoja na makampuni binafsi kama vile, Sea-Cliff Resort & Spa Ltd, Natures Land Safari’s & Rentals na Mbalageti Safari.

Kama ilivyo ada, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Irene F. M. Kasyanju  anashiriki maonyesho haya na tayari amekutana na wadau wote waliofika Uholanzi kuiwakilisha Tanzania. Wadau wengine wamekuja kibinafsi, kwa mfano, Makasa Tanzania Safaris, Kilidove Tours & Safari,s na DaMona Tanzania Safaris Ltd.

Hakika, hii ni fursa nyingine muafaka kwa Tanzania kujitangaza na kuzidi kuvutia wadau zaidi katika Sekta ya Utalii kuja kutembelea na kufanya biashara na Tanzania.